Friday, July 1, 2011

Tanzania kuanza kuchimba madini ya Urani

Duma
Duma wa Selou
Tanzania itaanza kuchimba madini ya urani katika mbuga ya wanyama ya Selous, eneo lililo chini ya udhamini wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughilikia mazingira maarufu kama World Heritage.
Akizungumza na Idd Seif wa Idhaa ya kiswahili ya BBC, Waziri wa maliasili na utali iwa Tanzania, Ezekiel Maige, alisema kuwa sehemu wanayohitaji kutumia kwa kuchimbia mgodi wa urani ni 0.69%,
hivyo kupunguza eneo la mbuga ya wanyama kwa chini ya 1%.
Kwa mujibu wa Waziri Maige, WHC imesema itatoa kibali iwapo tu masharti ya kutunza mazingira yatakuwa yamezingatiwa. Fedha zitakazopatikana kutokana na madini hayo zitasaidia kutunza
mbuga hiyo alisema Maige.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni UNESCO, hekta milioni tano la hifadhi ya mbuga ya Selou ina idadi kubwa ya Tembo, vifaru weusi, Chita, viboko na mamba na haijaharibu na
shughuli zozote za kibinadamu.
Katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Bw Maige alisema mradi huo bado uko katika hatua za mwanzo lakini utaathiri kwa asilimia 0.69 tu ya mbuga ya sasa na utakuwa ni chanzo muhimu
cha mapato ya nchi.
Makampuni yanatarajia kupata $200 milioni kwa mwaka kutokana na uchimbaji wa Urani na kati ya hizo $5 milioni zitalipwa kwa serikali ya Tanzania, alisema.
Sehemu ya mapato hayo itasaidia kutunza mbuga hiyo na mradi utatoa ajira kwa watanzania 1,600.
Katika mkutano wa mwaka wa kamati ya WHC, waziri Maige alisema, kulikuwa pia na wasiwasi kuhusu Msitu wa hifadhiwa Undendeule ulio kusini mwa mbuga ya Selou.
Lakini Bw Maige ambaye pia anashughulikia Utalii alisisitiza kuwa hakutakuwa na mathara kwenye msitu huo wa hifadhi ambao kwa sasa unaigharimu serikali $490,000 kwa mwaka kuutunza. Na
mapato yatakayotokana na uchimbaji wa madini hayo utasaidia kulipa askari wanaodhibiti ujangili.
Alisema Tanzania haikuhitaji kibali kutoka UNESCO ili kuendelea na mpango wake wa kuchimba Urani, lakini mataifa ya Afrika Mashariki yalitaka kujiridhisha na mapendekezo ya shirika hilo.
"mradi huu wa Urani utaanza," aliiambia BBC.
Aliongeza kuwa WHC Tanzania ifanye tathmini yenyewe itakayopitishwa na Tume ya Mazingira ya nchi hiyo.
Hatua ya pili ilikuwa ni hitaji la ujumbe wa wataalam kutoka UN kutembelea aeneo hilo na kutoa mapendekezo yake kuhusu kulinda na kutunza mfumo wa ekolojia.
Waziri alisema baada ya uamuzi huu taarifa itapelekwa katika mkutano mwingine wa WHC mwakani kuhusu mipaka ya Mbuga ya Hifadhi ya Selou.
Bw Maige aliongeza kuwa utafiti unaonyesha kuwa hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu sumu ya mionzi inayotokana na uchimbaji wa Urani katika eneo hilo.
"Kiwango cha mionzi kitabakia kuwa kile kile, haitakuwa na hatari kwa binadamu," alisema.

No comments:

Post a Comment