Thursday, July 7, 2011

CCM Kuanza Kusherehekea Miaka 50 Ya Uhuru

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Mwaka huu Sehemu ya nchi yetu, yaani Tanzania Bara itaadhimisha miaka hamsini ya Uhuru wake toka kwa Wakoloni. Uhuru huu uliopatikana miaka hamsini iliyopita ni kazi nzuri na ya Kizalendo iliyofanywa na Chama cha TANU.

Chama Cha Mapinduzi katika kukumbuka kazi hii nzuri ya kutafuta Uhuru wa nchi yetu kimeamua kufanya shughuli mbalimbali za kukumbuka kuzaliwa kwa chama kilicholeta Uhuru wa Tanzania Bara yaani TANU.

Itakumbukwa TANU ilizaliwa tarehe 7/7/1954 hapa Dar es salaam katika mtaa wa New street ambao kwa sasa unafahamika kama mtaa wa Lumumba mahali ambapo sasa ni  Ofisi Ndogo ya CCM Makao Makuu. Huo ukawa ndio mwanzo wa harakati za kudai Uhuru, Utu na Heshima ya Mwafrika katika nchi yetu.

Kwa kuienzi historia na kazi nzuri na ya Kizalendo iliyofanywa na TANU, Chama Cha Mapinduzi kimeamua katika kuadhimisha miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara kuandaa shughuli mbalimbali za kijamii zikiwa na kauli mbiu Uhuru na Kazi, kauli maarufu katika miaka ya nyuma ambayo Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere aliitoa katika hotuba yake ya kusisimua siku ya mkesha wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Mwalimu Nyerere aliitumia hotuba hiyo kuwaeleza wananchi wajiandae kuanza kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea wao wenyewe na nchi maenedeleo. Maadhimisho haya yatafanyika nchi nzima kuanzia ngazi za matawi na kuwashirikisha wanachama wetu na wananchi wote kwa ujumla. Shughuli zitakazofanyika ni kama zifuatavyo:-

     i.        Usiku wa kuamkia tarehe 7/7/2011 Vijana wa CCM nchini watakutana maeneo mbalimbali kufanya shamrashamra za kuzaliwa TANU

    ii.        Tarehe 7/7/2011 asubuhi wanachama wa CCM na wananchi watakutana kwenye matawi yao na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile, kufanya usafi, kusaidia ujenzi, kupanda miti, kutembelea wagonjwa mahospitalini n.k.

  iii.        Ikiwezekana kufanya matamasha mbali mbali yatakayowashirikisha vijana wasomi wanasiasa na wazee kujadili masuala mbali mbali yenye faida kwa Kata, Wilaya, Mkoa au Taifa kwa ujumla.

  iv.        Kufanya mikutano ya hadhara na kujikumbusha mafanikio yaliyopatikana kwa kila Mkoa na  Wilaya katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru.

Kwa Sehemu kubwa tunategemea walezi wa CCM wa Mikoa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa watashiriki shughuli hizo mikoani. Sherehe hizi zitaanza usiku wa tarehe 6/7/2011 kwa vijana wa CCM sehemu mbalimbali nchini kukutana na kusherehekea ikiwa ni pamoja na kufyatua MAFATAKI saa sita usiku ya siku hiyo, kama ishara ya kuzaliwa TANU.

Mwenyekiti wa CCM Taifa Dr. Jakaya M. Kikwete atashiriki sherehe hizi mkoani Dar es salaam, usiku wa Tarehe 06/07/2011 na tarehe 07/07/2011 asubuhi atakutana na Mabalozi wa Nyumba Kumi Mkoa wa Dar es salaam.

Ni mategemeo yangu vyombo vya habari vitashirikiana nasi katika kuuelimisha umma kuhusu historia hii muhimu ya Taifa letu na kutangaza matukio yote yatakayo ambatana na maadhimisho haya.

No comments:

Post a Comment