Friday, July 1, 2011

BARACK OBAMA NA MATUMAINI FEKI YA WAAFRIKA NA WEUSI

 
Mapema mwezi wa Juni, tarehe 3 mwaka huu, Barack Obama alifikia hatua kubwa katika harakati zake za kuteuliwa mgombea wa Chama cha Democratic. Ni hatua ambayo Wamarekani wanaiita (Nominee designate) mgombea mtarajiwa. Siku hiyo hapa Tanzania mkutano wa nane wa Taasisi ya Sullivan ulikuwa ukifanyika. Aliyewahi kujaribu harakati za kuchaguliwa, Mchungaji Jesse Jackson alinena kwa furaha akijivunia ni ushindi kwa weusi. Karibu waongeaji wote walizungumza juu ya hili kwa maono ya ushindi wa weusi.
Nikiwa kama mtanzania, mtu mweusi, nimefarijika pia kwa ushindi wa Seneta Barack Obama. Kufarijika kwangu si kwa mashiko ya rangi; yaani mweusi kashinda basi nami nifurahi. Kwangu nimeshangazwa karibu weusi wote wanamshabikia Obama eti kwa kuwa ni mweusi. Nina mashaka kama kweli hisia zetu zinaegemea zaidi rangi basi nadiriki kusema kuwa tusipokuwa makini nasi pia ni wabaguzi wa rangi wakubwa.
Nina wasiwasi: wote wanaouchukulia ushindi wa Obama kama ushindi kwasababu ni mweusi basi wamepotea njia. Ni lazima watu tufikiri kwa kina na si kushabikia tu ilihali inawezekana kabisa Obama hatakuwa na maslahi yoyote kwa waafrika na hata kwa watu weusi sehemu mbalimbali za dunia.

Labda niwarejeshe kwenye historia: Raisi wa zamani wa Marekani, Ruthirford Hayes aliwahi kunena kuwa “Us government is a government of the corporations, by corporations for the corporations”. Alimaanisha kuwa serikali ya Marekani ni serikali ya Makampuni, kwa maslahi ya Makampuni na inaendeshwa na Makampuni. Hapa alikuwa anajaribu kutanzua kiza kinene (illusion) kwenye maana ya demokrasia kama ilivyokuwa imeelezwa awali na mtangulizi wake Lincoln pale alipoweka maneno: “Government of the People for the People by the People” yaani: “serikali ya watu, kwa watu na maslahi yao” katika katiba ya nchi hiyo.

Ni katika msingi wa kuingalia serikali ya Marekani kama inayoongozwa na mtizamo wa Katiba kuheshimiwa bila ubazazi wa aina yeyote kama tunavyoshuhudia hapa kwetu, basi kama Obama atachaguliwa kuwa raisi wa Marekani tujue kabisa atafanya kazi kwa misingi ya Rais wa zamani Ruthirford Hayes. Hapa ndipo panaponifanya nisiwe na matumaini kama kweli mtu mweusi kuwa Rais wa Marekani basi tutafaidika na lolote tofauti na marasi wengine weupe waliokwishapita na kutawala Marekani. Ni vyema tumfurahie Seneta Obama kutokana na wajihi wake: ni jinsi gani ameweza kuchambua masuala mbalimbali kwa ufasaha na kuonesha jinsi gani anavyoweza kufikiri. Ni kigezo hiki tu naweza kufurahia ushindi wa Obama na wala kamwe si rangi yake. Kinyume na hapo naona ni mtizamo wa kibaguzi ambao hauna nafasi katika dunia ya kileo.

USHINDI HARAKATI ZA MTU MWEUSI

Kuna wengine wanauona ushindi wa Seneta Obama kama vile ni ushindi wa harakati za kutafuta haki za mtu mweusi. Hebu nikumbushie harakati za kumkomboa mtu mweusi nadhani zilianza siku nyingi chini ya watu kama akina Willium Du Bois, Marcus Garvey, George Padmore, Malcolm X, Martin Luther King, Nelson Mandela, Julius Nyerere, Jomo Kenyatta, Kenneth Kaunda, Robert Nesta Marley hadi akina Jesse Jackson na Luis Farhani wa leo hii Marekani.

Nimejaribu kupiga picha na nimeona hadi leo hii mtu mweusi kafikia mafanikio mengi katika nyanja nyingi. Kwa mfano, miongo mitatu iliyopita tunaweza kung’amua mafanikio ya mtu mweusi kama ifuatavyo:
Mosi, mwishoni mwa miaka ya 1970, waafrika weusi wa Marekani waliweza kutawala fani ya muziki kimataifa pale mziki aina ya kufokafoka ulikuwa sana kuanzia New York na kuua kabisa muziki wa Rock uliokuwa ukitawala.
Pili, baada ya mafanikio ya muziki, mwafrika asilia alianza kuonesha mafanikio duniani katika mchezo wa soka. Mwaka 1990, timu ya Taifa ya soka ya Cameroon (Indomitable Lions) ilifikia hatua ya robo fainali ya Kombe la dunia kule Italia chini ya Roger Milla. Baadaye mwaka 2002 kule Korea na Japan timu nyingine ya Senegal nayo ilifika hatua kama hiyo.

Jambo la tatu, katika miaka hiyo hiyo ya 1990, kule Afrika ya Kusini, Nelson Mandela na wafungwa wenzake kama akina Govan Mbeki, Walter Sisulu waliachiwa huru. Baadaye mwaka 1994 waafrika walio wengi wakafanikiwa kuunda serikali ndani ya nchi ambayo walinyimwa haki hiyo kwa miongo kadhaa. Si hapa Afrika tu mtu mweusi kafanikiwa, kwa mfano, mwaka 1997, kijana mweusi wa Marekani: Eldrick ‘Tiger’ Woods akaweka historia kushinda mashindano makubwa ya mchezo wa gofu “US Masters” na ametawala mchezo huo kidunia hadi ninapoandika makala hii. Mchezo wa kikapu ndio usiseme, mtu mweusi katawala hasa.

TIJA YA MAFANIKIO YA MTU MWEUSI

Kwa ujumla mtu mweusi kafanikiwa sana kwa miaka ishirini iliyopita si kwenye fani ya sanaa na michezo tu. Bali hata kwenye mambo ya uongozi wa taasisi nyeti za kimataifa, mwafrika tayari anajivunia kuweza kuongoza katika nyadhifa za juu kabisa. Kwa mfano, Umoja wa Mataifa (UN) , mwaka 1991 – 1994 ulikuwa chini ya Butros Butros Ghali raia wa Misri, baadaye akarithiwa na mweusi hasa Koffi Atta Annan wa Ghana mwaka 1995. Ni kipindi hichohicho, Jumuiya ya Madola ilikuwa chini ya Chief Emeka Anyaoku wa Nigeria kama Katibu Mkuu. Haya yote ilikuwa ni kuionesha dunia kuwa mtu mweusi anaweza na anatambulika. Lakini tujiulize: Je kulikuwa na msaada gani mkubwa kwa waafrika pale yote haya yalipojitokeza? Nakumbuka tulifurahi na kushangilia kutokana na hisia zenye mashiko ya rangi.

Watu wengine wanaweza kujiuliza labda mafanikio mengi ya mtu mweusi niliyoyaelezea hayakutokea Marekani bali hapa Afrika chini ya waafrika. Lakini kwa sasa yanatokea kule Marekani, ambalo ndilo Taifa linalotoa mwongozo wa dunia basi hatuna budi kuwa na matarajio. Na hii ndio hisia ninayoiona miongoni mwetu wengi kama “matumaini feki”. Kwangu siamini hivyo na kamwe sitaamini. Labda nikumbushie tu pale Raisi George Bush alipoingia madarakani na kumteua Collin Luther Powel kama mweusi wa kwanza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, yaani cheo cha juu kabisa baada ya Raisi na Makamu wake Marekani. Raisi Bush alimteua baadaye mweusi mwingine Condoleza Rice katika nafasi hiyo ya juu kabisa hadi wakati naandaa makala hii.
Pia ni miaka si chini ya mitatu iliyopita, mwafrika mzaliwa wa Uganda John Sentamu alichaguliwa kuwa Askofu wa jimbo la York huko Uingereza. Hii ni nafasi ya pili kwa cheo ndani ya kanisa la Anglikana duniani. Katika haya yote yanayohusu ukombozi wa mwafrika ni mafanikio ambayo wanaharakati wanatumia mara nyingi neno la kiingereza “African Renaissance” yaani kuzaliwa upya kwa mwafrika.
Kwangu hili naliona pia kwa mtizamo huo kwani mwafrika ameweza kuondokana na kadhia za kibaguzi za zamani. Lakini tujiulize swali: Hivi mafanikio yote hayo yamesaidiaje weusi wa dunia hii? Tuache ukichaa, hebu angalia hata kule Afrika ya Kusini sasa mtu mweusi anapinga mweusi mwenzake kuishi nchini mwake. Umasikini wa mtu mweusi uliosababishwa na ufisadi wa wanaharakati wa zamani umetufikisha hapa tulipo. African Reinassance imepoteza mwelekeo huko Afrika Kusini kwa Madiba. Yote ni kwasababu mtu mweusi amekubali awe mtumishi na wakala wa mfumo wa kiutawala wa aina ya: “ corporate by corporation for the corporation”. Akina Raisi Mbeki na wapigania uhuru wenzake wamegeuka umma wa weusi na kuacha kuwatumikia na kuyatumikia makampuni.

Vivyo hivyo, nadhani hata Seneta Barack Obama atafuata mwelekeo huohuo kwa kuitumikia katiba ya Marekani ambayo imejaa lugha ya giza ikimaanisha mambo ambayo kimatendo ni kinyume na maneno. Yaani ikifuata mwelekeo wa Raisi Hayes badala ya ule sahihi wa Lincoln.
Ndio maana nilishangazwa sana mara baada ya Obama kuthibitisha kuwa ni mgombea mtarajiwa, hotuba yake ya kwanza mjini Washington ilikuwa ni mbele ya umati wa watu 7000 uliojumuisha “Kamati ya Mambo ya Waisraiel – Wamarekani ( Jewish American Israel Public Affairs Committee – AIPAC. Tujiulize ikiwa weusi wengi ndio waliompigia kura ilikuwaje aanze na shukrani kwa Wayahudi?

Dhahiri mwelekeo hapa wa dunia lazima tutumie bongo kufikiri na si kufuata hisia tu. Barack Obama hana njia nyingine ila ataungana na wale wengine niliowataja awali kama alama ya “African Reinassance” ambao wamemtangulia katika kuwatumikia wazungu. Kwani katika demokrasia ya leo, ule mtizamo wa Raisi Lincoln ndivyo sivyo. Mambo ya ‘Serikali ya watu, kwa watu na maslahi yao’ ni hadithi ya alinacha. Democrasia leo ni kutumikia makampuni makubwa yenye ushawishi. Haya ndiyo yenye kupenyeza rupia kusaidia kampeni za akina Seneta Obama ili wayatumikie pindi watakaposhinda. Ni kama vile hapa kwetu Tanzania vigogo fulani walivyojiundia vikampuni kwa mgongo wa EPA ili kupata fedha za kampeni. Obama yeye hakutumia mbinu za kibazazi za kujiundia vijikampuni feki ila anafadhiliwa na makampuni ambayo lazima alipe fadhila.

Mwisho, Seneta Obama ataungana na waliomtangulia: Koffi Annan, Colin Powel, Condoleza Rice, Chief Emeka Anyaoku na hata mama yetu mpendwa Asha Rose Migiro ambao walitumika na wengine wanatumika kwa sasa kama kielelezo feki cha kioo cha ubinadamu wa serikali za Marekani na Ulaya kukubalika ulimwenguni mbele ya umma wa watu weusi. Kwa mtizamo wangu huu ni lazima wale wote wenye mawazo kuwa Obama atasaidia weusi na hasa sisi waafrika waandike maumivu na masikitiko. Kwani akishakuwa Rais, kipaumbele kitakuwa ni maslahi ya Marekani kwanza kwa kufuata maneno ya Raisi Rutherford Hayes. Yaani kutumikia makampuni mbalimbali kabla ya kutumikia wapiga kura. Je tutarajie kama Raisi wa Marekani hatumikii watu wake, je atatumikia watu walio mbali naye kama sisi waafrika? Tuache ubaguzi tufikiri sana na tuangalie kwa bongo zetu na si kwa mioyo.

No comments:

Post a Comment