Friday, July 1, 2011

KUMBUKUMBU YA DKT MARTIN LUTHER KING JR NA TAFAKURI KUHUSU "I HAVE A DREAM" YA NYERERE (MAKALA KATKA GAZETI LA "MTANZANIA" LA LEO

Powered by Translate


Siku chache zilizopita Wamarekani waliadhimisha siku ya Dakta Martin Luther King Jr,mmoja wa wapigania haki za Waamerika Weusi.Historia inamkumbuka Dkt King (aliyezaliwa mwaka 1929 na kuuawa kwa risasi mwaka 1968)kama nguzo muhimu katika kupigania haki za Waamerika Weusi nchini humo.Pengine kilichomfanya wanaharakati huyo akubalike zaidi ni imani yake ya kudai haki kwa njia za amani.

Miaka mitano kabla ya kuuawa,mwaka 1963,Dkt King alitoa hotuba ambayo hadi leo imeendelea kuwa na mvuto mkubwa sio nchini Marekani pekee bali pia sehemu mbalimbali duniani katika mapambano ya kudai usawa.Katika hotuba hiyo iliyopewa jina “I Have a Dream” (“Nina Ndoto”,kwa tafsiri isiyo rasmi),Dkt King alieleza matamanio yake kuona Waamerika Weusi na Weupe wakiishi pamoja kwa amani na usawa.Hotuba hiyo iliyotolewa mbele ya watu zaidi ya laki mbili,inakubalika miongoni mwa wengi kama moja ya hotuba za muhimu kabisa katika historia ya Marekani.Mwaka 1999,hotuba hiyo ilichaguliwa na wasomi kuwa ni hotuba bora kabisa za karne ya 20.

Miongoni mwa nukuu muhimu katika hotuba hiyo ni pamoja na (kwa tafsiri yangu isiyo rasmi) “…nina ndoto kwamba siku moja taifa hili litasimama na kuishi kama inavyotamkwa kwenye imani yake….nina ndoto kwamba siku moja watoto wangu wanne wataishi katika taifa ambalo hawatahukumiwa kutokana na rangi ya ngozi zao bali tabia/utu wao….nina ndoto kwamba siku moja watoto wa waliokuwa watumwa na watoto wa waliokuwa wamiliki watumwa watakaa pamoja katika meza ya undugu…”

Msukumo uliotokana na uongozi wa harakati za Dkt King ulisaidia sana kubadili historia ya Marekani hususan usawa kwa (Wamarekani) Weusi, na kupelekea mabadiliko mbalimbali dhidi ya sheria za kibaguzi.Miongoni mwa sheria hizo ni pamoja na “Civil Rights Act” ya mwaka 1964 iliyoharamisha ubaguzi kwenye sehemu mbalimbali katika jamii.Mwaka uliofuata, “Voting Rights Act” ilipitishwa na kufuta kipengere kilicholazimisha wapiga kura watarajiwa kufanya testi za kupima uwezo wa kusoma na kuandika (wengi wa waathirika wa kipengere hicho walikuwa Wamarekani Weusi ambao walikuwa na maendeleo duni kielimu kutokana na kubaguliwa).

Maadhimisho ya siku ya Dkt King yamekuwa yakitoa changamoto nzuri kwa jamii ya Wamarekani kutafakari mahusiano kati ya Weupe na Weusi.Wengi hujiuliza iwapo ndoto za Dkt King zimetimia kweli,zinaelekea kutimia au hazina dalili ya kutimia kabisa.Ni maswali magumu ambayo yanahitaji uchambuzi wa kina kuyajibu,na pengine hata kwa uchambuzi wa kina bado inaweza kuwa vigumu kupata jawabu moja linalokubalika.Kingine kinacholeta ugumu wa kupata jawabu ni tofauti ya vizazi.Kwa walioishi nyakati za ubaguzi wa rangi na kushuhudia harakati za Dkt King wanaweza kuwa na mtizamo tofauti kuhusu kutimia kwa ndoto za mwanaharakati huyo ukilinganisha na kizazi cha hivi karibuni ambacho kinamwelewa Dkt King kupitia kumbukumbu za historia tu.

Hata hivyo ni rahisi kukubaliana kwamba harakati za Dkt King na wenzie zimesaidia kuleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na hayo ya kisheria niliyotaja awali.Wapo wanaokwenda mbali zaidi na kutoa mifano ya mafanikio ya Waamerika Weusi maarufu kama Jenerali Colin Powell na Condoleeza Rice ambao wameshika nafasi nyeti katika uongozi wa taifa hilo.Lakini mfano mzuri zaidi ni Barack Obama,seneta Mweusi anayewania kuteuliwa kugombea urais wa nchi hiyo kupitia chama cha Democrats.Akiteuliwa kuwa mgombea,ataweka historia ya pekee nchini humo,na akifanikiwa kushinda urais basi hiyo itakuwa zaidi ya kuweka historia (tuite kuandika historia upya).Hata kama atashindwa,mafaniko aliyokwishafikia hadi sasa ni hatua muhimu katika kutimia kwa ndoto za Dkt King.

Afrika nayo imetoa akina Dkt King kadhaa,na kwetu Tanzania tunajivunia Baba wa Taifa marehemu Julius Nyerere ambaye (kama Dkt King) alikuwa na ndoto zake kadhaa ambazo kimsingi zilihusu kuwa jamii yenye usawa.Ndoto za Mwalimu zilivuka mipaka ya Tanzania kuhakikisha kuwa Afrika yote inakuwa huru.Mchango wa Mwalimu katika mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika utaendelea kukumbukwa milele.Na pengine hapo ndipo baadhi yetu tunagundua mabadiliko ya vizazi yanavyochangia kusahaulisha historia.

Mara nyingi napokutana na vijana Waafrika wenzangu (wanaoishi hapa Uingereza) kutoka nchi kama Zimbabwe,Zambia,Angola,Msumbiji,Afrika Kusini,Namibia na Uganda,nabaini kwamba wengi wao aidha wamesahau au wanapuuza mchango wetu katika ukombozi wa nchi zao (kwa Uganda ni kumng’oa Nduli Idi Amini).Angalau Wazimbabwe wanaweza kuwa na kisingizio kwamba kutokana na ubabe wa Mugabe,baadhi yao wanaweza kutoona faida ya kumkimbiza mkoloni na kujipatia uhuru.

Lakini pengine si busara sana kuwalaumu wanaopuuza mchango wa Mwalimu na Tanzania kwa ujumla katika ukombozi wa nchi zao kwani inawezekana kabisa wanafuatilia kinachoendelea nchini mwetu na kugundua kwamba baadhi yetu tumetupilia mbali kabisa jitihada za Baba wa Taifa kuhakikisha tunajenga jamii yenye usawa.Kwa vile dunia ni kama kijiji,katika zama hizi za utandawazi,majirani zetu hao watakuwa wanasoma na kusikia habari kuhusu ufisadi nchi mwetu,na pengine kubaki wanajiuliza “hivi hawa si ndio waliokuwa wanapigania usawa barani Afrika?Mbona wenyewe wako sasa wanafanyiana hivi?”.

Mwalimu alifariki huku baadhi ya ndoto zake zikiwa hazijatimia.Wachambuzi wazuri wa siasa wanadai kwamba baadhi ya ndoto hizo zilishindikana hata kabla hajang’atuka (kwa mfano upinzani wake wa awali dhidi ya ushirikiano na mashirika ya fedha ya kimataifa).Lakini nadhani Mwalimu aliumia zaidi kuona Azimio la Arusha likizikwa hai na Azimio “la kimyakimya” la Zanzibar (naliita hivyo kwani sijawahi kuona “document” yoyote rasmi inayoelezea kilichomo kwenye Azimio hilo).

Wakati Dkt King anaweza kufarijika huko aliko iwapo angeweza kufahamu baadhi ya mambo yanayoendelea sasa nchini Marekani (hususan kuhusu Obama) nashindwa kuhisi ni lipi litakalokuwa linampa furaha Mwalimu huko aliko tukiweka pembeni suala la amani na utulivu.Na hata katika hilo (la amani na utulivu) wapo wanaodai kuwa ni ya kufikirika zaidi kwani ni ukweli usiopingika kwamba masikini ni wengi zaidi kuliko matajiri,na yayumkinika kusema kwamba matumbo ya masikini hao hayana amani wala utulivu.

Kadhalika,kuna wanaodai kwamba kigezo cha amani na utulivu kimekuwa kikitumiwa vizuri zaidi na mafisadi wanaoamini kwamba Watanzania ni wapole sana na hawako tayari kuchezea lulu ya amani na utulivu kwa vile tu flani kakwiba mabilioni ya umma.Pengine mafisadi hao wako sahihi kwani tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watu wakiua,wakapewa dhamana za chapchap na kuendela na maisha yao kama kawaida huku hatima ya kesi zao ikisubiri isahaulike akilini mwa watu.Wakati hayo yakitokea,magereza yetu yamejaa wamachinga wanaotafuta ridhiki mitaani na wafungwa wengine ambao inawezekana kabisa walijiingiza kwenye wizi wa nyanya au kuku kwa vile tu hawakuwa na njia nyingine ya kujipatia kipato.Uhalifu ni uhalifu,na kila mhalifu anastahili adhabu lakini inatatiza kuona wahalifu wengine wakiendelea kula raha kana kwamba waliyofanya si kinyume cha sheria.

Tofauti kubwa kati ya ndoto ya Dkt King na Mwalimu ni kwamba wakati Wamarekani Weusi wanafanya kila jitihada kuenzi jitihada za Dkt King kwa kuendeleza mapambano dhidi ya ubaguzi na kupigania usawa,sie tuko kwenye mgawanyiko mkubwa kati ya wachache walionacho wasiosubiri kuongezewa bali wanapora, na wengi wasio nacho ambao hata kile kidogo walicho nacho kinaporwa.Hili ndio tishio kubwa,sio tu kwa ndoto za Mwalimu,bali hata kwa hiyo lulu yetu ya amani na utulivu.

No comments:

Post a Comment