Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amejibu hoja zilizotolewa na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, wiki iliyopita kuwa serikali ya awamu ya nne imeshindwa kufanya maamuzi magumu, kwa kuorodhesha mambo mbalimbali ambayo yamesema ni magumu yakiwa yamechukuliwa na serikali.
Pinda alisema hayo alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, bungeni, mjini hapa jana jioni. Lowassa akichangia mjadala wa bajeti hiyo wiki iliyopita, alisema kuna ugonjwa wa kuogopa kutoa maamuzi hivyo akataka serikali kutoa maamuzi na kusema:
“Heri ukosee kwenye kutoa maamuzi kuliko kutotoa maamuzi. Toeni maamuzi, acheni kuogopa, tumepewa nchi, tufanyeni maamuzi. Heri uhukumiwe kwa kutoa mamuzi kuliko kwa kutotoa maamuzi. Toeni maamuzi. Nasema tunaweza kufanya. Tukinuia, tukiamua, tunaweza kufanya.”
Pinda alisema serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Dk. Jakaya Kikwete ndiyo pekee imefanya maamuzi magumu na mazito kuliko serikali zote zilizopita.
Alisema imekuwa ikifanya maamuzi thabiti na magumu, lakini kwa busara na tahadhari ili kutenda haki na kwa kuzingatia uwezo wake ili kulinda maslahi ya wananchi na kudumisha amani.
Alisema katika kufanya maamuzi hayo, serikali imekuwa makini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Aliyataja maamuzi magumu yaliyokwishafanywa na serikali ya awamu ya nne kuwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani waliokuwa mawaziri wa serikali zilizopita kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili za kutumia madaraka isivyo halali; na pia kujenga shule za sekondari za kata, ambazo zimewezesha wanafunzi wengi kupata elimu ya sekondari.
Mengine ni kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom); kujenga Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo; kukamilisha miradi yote 27 ya barabara kuu zilizoanzishwa na serikali ya awamu ya tatu; ujenzi na ukamilishaji wa miradi ya maji nchini; na kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Pia, kuondoa mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ); kupanua na kushamiri kwa demokrasia nchini kwa kiwango kikubwa; uhuru mkubwa wa vyombo vya habari; na kuruhusu kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya.
“Lakini pia katika awamu hii ndipo tumefanya maamuzi mazito sana ya kuvunja Baraza la Mawaziri kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Edward Lowassa. Hili nalo halikuwa jambo jepesi hata kidogo. Inataka Moyo!” alisema Pinda.
Aliongeza: “... maisha ya serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa dhana ya uwajibikaji wa pamoja kupitia Baraza la Mawaziri. Tunachohitaji ni kuvumiliana. Kuvuta subira, kwani mambo mema hayataki haraka! Tutaamua na Tutafanya!”
Akizungumzia suala la posho, alisema suala hilo ni muhimu kutazamwa kwa upana wake na kwa msingi ulioelezwa chini ya Mpango wa Miaka Mitano, yaani kuzungumzia posho zote.
“Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Waraka wa Masharti ya Kazi za Mbunge; stahili za wabunge ni pamoja na zifuatazo: Mshahara wa mbunge kodi Sh. 588,000 ambao ulishakatwa, ambao haujakatwa kodi ni Sh. 2,305,000, ukisakatwa kodi ni Sh. 1,717,000. Posho ya ubunge; posho ya vikao vya Bunge na kamati zake,” alisema Pinda.
Aliongeza: “Posho ya madaraka kwa viongozi; Entertainment Allowance (posho za maburudisho) kwa viongozi; posho ya kujikimu ndani na nje ya nchi; posho ya mavazi anaposafiri nje ya Tanzania; posho ya msaidizi wa ofisi ya mbunge; posho ya usafiri wakati wa vikao vya kamati na mikutano ya Bunge; vilevile, kuna posho ya mafuta (Lita 1,000) kwa mwezi na Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo (CDCF).”
Pinda alisema kwa kuwa suala hilo lipo ndani ya Mpango wa Maendeleo, serikali italitafakari kwa undani na kuangalia posho zipi hazina tija na zipi zina tija na manufaa ya kuongeza ufanisi ili ikiwezekana zihuishwe na kujumuishwa ndani ya mishahara au vinginevyo kama itakavyoonekana inafaa.
Alisema serikali pia itaangalia suala la kupunguza gharama za matumizi ya serikali kwa ujumla wake ikijumuisha kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika taasisi zote za serikali.
Pinda alisema kwa maelekezo ya Rais Kikwete, uamuzi wa kuhamia Dodoma hauna budi kutekelezwa na kusisitiza kuwa hata kama fedha zimetengwa, Ofisi ya Waziri Mkuu itajengwa Dodoma.
No comments:
Post a Comment