Wednesday, June 29, 2011

Wasifu: Osama bin Laden

Siku ambayo ndege zilizotekwa nyara ziligonga majengo ya World Trade Centre na makao ya wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, ni vitendo vilivyombadilisha Osama bin Laden kutoka mtu mdogo asiyejulikana na kumfanya kuwa mojawapo watu wanaotambulikana sana duniani.
Osama bin Laden, katika mojawapo ya picha enzi za uhai wake.

Lakini alipojaribu kuepuka juhudi za Marekani kumkamata aliendelea kuwa kitendawili. Mawasilianao yake na dunia yalikuwa zaidi kwa kanda za video kupitia kituo cha televisheni cha Al Jazeera.
Bofya SIKILIZA WASIFU WAKE
Bin Laden aliwahi kunukuliwa akisema: "Kile ambacho Marekani inakionja hivi leo ni kitu kidogo sana ikilinganishwa na kile ambacho tumekuwa tukikipata katika miongo kadhaa. Taifa letu limekabiliwa na hali hii ya kudhalilishwa na kudharaualiwa kwa zaidi ya miaka 80. Wanawe wanauwawa, damu yao inamwagwa, maeneo yake matakatifu yanahujumiwa na hayatawaliwi kwa mujibu wa amri zake Mwenyezi Mungu."
Osama bin Laden alizaliwa mwaka 1957 katika familia yenye utajiri mkubwa. Baba yake alianzisha kampuni kubwa ya ujenzi katika Saudi Arabia. Akiwa ni miongoni mwa ndugu 18 wa kiume, Osama aliwahi kufanya kazi katika biashara hiyo ya familia. Maisha yake yalianza kubadilika alipokuwa kijana pale Muungano wa Sovieti ulipoivamia Afghanistan.
Alipokwenda Aghanistan, Osama alikuwa kijana sana ambaye alitaka kujijengea umaarufu, katikati ya vita vitakatifu. Osama bin Laden alikaa kwa kipindi cha takriban miaka 10 nchini Afghanistan, na kuanzisha fungamano na wanaharakati wa siasa kali za kiislamu kote duniani.
Na baada ya majeshi yaliyovunjika moyo ya Sovieti kuondoka Afghanistan mnamo mwaka 1989. Osama bin Laden alirejea nyumbani Saudi Arabia. Mwaka mmoja baadaye alijitolea kumpa msaada wa kijeshi mfalme Fahad wakati Iraq ilipoivamia nchi jirani ya Kuwait. Lakini Osama alipatwa na mshtuko mkubwa pale Mfalme Fahad alipokataa toleo lake na badala yake kuigeukia Marekani.
Osama alinyaganywa uraia wa Saudi na akarejea Afghanistan ambayo wakati huo ikitawaliwa na Wataliban ambao alikubaliana nao kuhusu tafsiri ya uislamu.
Mnamo mwaka 1998 aliwahimiza waislamu wawauwe Wamarekani mkiwemo raia popote pale watakapowapata, kukafuatiwa mashambulio kadhaa ikiwa ni pamoja na dhidi ya balozi za Marekani katika Kenya na Tanzania na manowari ya USS Cole katika mwambao wa Yemen. Halafu shambulio la September 11, 2001.
Nyumba ya ghorofa ambamo bin Laden anaaminika alikutwa na kuuawa.

Osama bin Laden aliwasifu waliofanya shambulio hilo. Rais Bush akasema atasakwa apatikane akiwa hai au mfu.
Rais Bush alikunukuliwa kusema: "Sijui kama tutampata kesho au mwezi ujao au mwaka ujao. Lakini hapana shaka tutampata tu."
Ingawa Waislamu wengi walilaani vifo vya watu katika miji ya New York na Washington, Osama bin Laden alichukuliwa na wengi kuwa ni shujaa, aliyetetea haki za Wapalestina na kupinga nguvu za Marekani.
Alioa mke wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 17 na baadaye akawaoa wake wengine wanne. Osama bin Laden anaaminika kuacha watoto 17.

No comments:

Post a Comment