Tuesday, June 28, 2011

Simba kumuuza Okwi mil. 150/-



UONGOZI wa klabu ya Simba umesema upo tayari kumuuza mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi kwa klabu yoyote kwa kitita cha dola 100,000 za Marekani (sh. milioni 150).
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, hawaoni tatizo kumuuza Okwi, lakini lazima klabu inayomuhitaji iwe tayari kulipa kiasi hicho cha pesa.
Msimamo huo wa Simba umekuja siku chache baada ya kuwepo na taarifa kwamba, African Lyon imekuwa ikihaha kumsajili mshambuliaji huyo kutoka Uganda.
Rage alisema ameshangazwa kusikia kuwa, viongozi wa African Lyon wameshaanza kufanya mazungumzo na mchezaji huyo bila ya kupata ridhaa ya viongozi wa Simba, jambo alilodai ni kinyume na taratibu za usajili.
"Kwa kweli nawashangaa sana hawa African Lyon, kama wanatumwa au wana nia nzuri, waje kwetu kuomba kuzungumza na mchezaji huyo na wakikubaliana naye, watulipe dola 100,000 tuwape Okwi,"alisema Rage.
Rage alisema anahisi viongozi wa African Lyon hawafahamu vyema sheria na kanuni za usajili, hivyo amewataka wazisome na kuzielewa vyema katika kipindi hiki cha usajili.
"Sisi hatukatai kumuuza Okwi, kama wana ubavu waje na dola 100,000, kinyume na hapo haiwezekani na kama wamempa pesa zao, wajue wazi kamba wameliwa,”alisisitiza.
Kwa mujibu wa Rage, mchezaji huyo ana mkataba na Simba hadi mwaka 2012, hivyo kama kuna klabu inayotaka kumsajili, italazimika kuvunja mkataba wake.
Akizungumzia usajili wa Simba kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, Rage alisema unaendelea vizuri na kuongeza kuwa, wamepanga kutumia sh. milioni 375.
Alisema kazi ya usajili wa wachezaji wapya inafanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope na kusisitiza kuwa, ana imani kikosi cha timu hiyo msimu ujao kitakuwa tishio zaidi ya Yanga.

No comments:

Post a Comment